#Football #Sports

VILLA WAITANDAZA BOLOGNA KUWEKA MIADI NA FOREST

Klabu ya Aston Villa ilijikatia tiketi ya nusu fainali ya michuano ya UEFA UROPA League ambako watamenya na Nottingham Forest katika pambano litakalokutanisha klabu hizo za EPL baadaye mwezi huu.

Hii ni kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Bologna jana usiku na kufikisha ushindi wa jumla ya mabao 7-1 kutokana na ushindi wa mabao 3-1 katika mkondo wa kwanza wa robo fainali.

Vijana hao wa Unai Emery wanaopigiwa upato wa kutwaa taji hilo, walionyesha mchezo wa aina yake chini ya mkufunzi wao ambaye ameshinda taji hilo mara 4 na kupiga hatua kubwa katika azma yao ya kutamatisha kipindi cha miaka 30 bila taji lolote.

Villa walihitaji dakika 16 pekee kuchukua uongozi kwenye mechi ya jana, Ollie Watkins ambaye sasa ameifungia klabu hiyo ya Uingereza mabao 100 akiwaweka kifua mbele.

Morgan Rodgers alipoteza nafasi ya kufunga la pili mkwaju wake wa penalti ulipopanguliwa na kipa Federico Ravaglia kutokana na handiboli.

Hata hivyo, mabao kutoka kwa Emiliano Buendia, Ezri Konsa na Rodgers yaliihakikishia Villa ushindi huo mnono na kuweka miadi na Forest ambayo itakuwa ni semi fainali ya kwanza kuzikutanisha klabu za Uingereza tangu Manchester United na Arsenal walipomenyana katika semi fainali ya kombe la klabu bingwa bara Ulaya msimu wa 2008-2009.

Kwa upande wao, Forest waliilaza Porto jumla ya mabao 2-1 katika mikondo miwili kufuatia ushindi wa bao 1-0 jana usiku kutinga nusu fainali ya mashindano ya bara Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1984.

Baada ya sare ya bao 1-1 kwenye mkondo wa kwanza wiki jana, Morgan Gibbs-White alifunga bao la pekee la mchezo jana usiku dhidi ya Porto waliosalia 10 uwanjani kufuatia kadi nyekundu kwa Jan Bednarek katika dakika ya 8.

Semi fainali nyingine itawakutanisha Freiburg na Braga ambao pia walifuzu jana usiku.

Freiburg waliilaza Celta Vigo mabao 3-1 na kufuzu kwa jumla ya mabao 6-1, nao Braga wakaicharaza Real Betis jumla ya mabao 5-3 kufuatia ushindi wa mabao 4-2 jana usiku.

Imetayarishwa na Antony Nyongesa

VILLA WAITANDAZA BOLOGNA KUWEKA MIADI NA FOREST

JUNIOR STARLETS WAREJEA

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *