MATUMAINI YA KIKOSI CHA X-COUNTRY MAREKANI
Wanariadha wa Kenya watakaowakilisha taifa katika mashindano ya ubingwa wa Cross Country mwaka huu yatakayoandaliwa Jumamosi hii eneo la Tallahassee katika jimbo la Florida nchini Marekani wameelezea matumani ya kutetea ubingwa wa taifa kwenye mbio hizo.
Licha ya mashindano hayo kutawaliwa na wanariadha binafsi wa Uganda, Kenya inajivunia ubingwa wa mbio hizo kwa jumla ulioandikishwa mwaka jana jijini Belgrade nchini Serbia, ambako iliongoza kwa nishani, ikijizolea jumla ya medali 11 zikiwemo dhahabu 6, fedha 2 na shaba 3.
Mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 10 Agnes Ng’etich, ataongoza kampeni hizo kwa upande wa wanawake waliokolea, akisaidiwa na kikosi cha wanariadha wenza Maurine Chebor, Brenda Kenei, Rebecca Mwangi, Joyline Jepkemoi na Caren Chebet.
Kwa upande wa wanaume waliokolea, mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 10,000 mwaka wa 2023 Daniel Ebenyo, ataongoza kikosi cha Kenya katika kuwinda nishani zaidi na ubingwa kwa wanariadha binafsi.
Wengine ni Ishmael Rokitto, Robert Koech, Edwin Bett, Weldon Langat, Dennis Kemboi, Kevin Chesang, Shadrack Koech na Daniel Munguti.
Vikosi vya wanariadha walio chini ya umri wa miaka 20 pia vitashiriki.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 

































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































