GOR MAHIA WATISHIA WAPINZANI WA KICHAPO
Mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu ya soka nchini, KPL, Gor Mahia, wametangaza ubabe wao wa soka na dhamira ya kutwaa tena taji hilo kutokana na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sofapaka ugani Nyayo Jumamosi.
Baada ya tahadhari katika dakika za ufunguzi, Gor walichukua udhibiti wa mechi, wakinyakua uongozi kupitia Frank Odhiambo, Sylvester Owino na kisha kujihakikishia pointi zote 3 kupitia kwa Ebenezer Adukwaw, mabao yote yakifungwa katika kipindi cha kwanza.
Ushindi huo sasa umeimarisha uongozi wao wa ligi, wakiwa na pointi 40 baada ya mechi 19, pointi 4 mbele ya wapinzani wao wa karibu AFC Leopards ambao wamecheza mechi 18.
Licha ya ushindi huo mnono ulioonekana rahisi, kocha mkuu wa Gor Mahia Charles Akonnor, amewaonya vijana wake dhidi ya kulegeza kamba.
Katika matokeo mengine, Mara Sugar walikataa kupigwa ugenini dhidi ya Kakamega Homeboyz ugani Bukhungu, wakitoka chini mara tatu na kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Katika uwanja wa Kasarani, KCB FC walijikung’uta vumbi la Mathare, wakitoka chini 1-0 na kupata ushindi wa mabao 2-1.
Baada ya kujifunga bao mapema, wanabenki hao walijizatiti na kusaka njia ya kurejea mchezoni kupitia December Kisakah na Amatton Samunya.
Katika matokeo mengine, Shabana FC hatimaye waliandikisha ushindi nyumbani, baada ya kuwacharaza wageni wao Bandari FC bao 1-0, huku Murang’a Seal wakiendeleza rekodi ya matokeo bora, mara hii waathiriwa wao wakiwa APS Bomet waliorambishwa kichapo cha mabao 2-1.
Huku ligi hiyo ikiingia hatua muhimu, Gor wameendelea kujiimarisha uongozini, KCB FC ikianza kujikita miongoni mwa wawaniaji wa ubingwa huku timu zinazokabiliwa na shoka la kushushwa daraja zikiendelea kuweka juhudi za kujiokoa.
Leo hii ni zamu ya bingwa mtetezi Police FC dhidi ya Bidco United, chombo cha maafande hao kikiendelea kutikiswa na mawimbi.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 











































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































