SHUJAA WATUZWA NA ‘KUNDI GUMU’ UBINGWA HONG KONG 7S
Timu ya taifa ya raga ya wachezaji 7 kila upande, Shujaa, watakabiliwa na mtihani mgumu wa msimu wao baada ya kuwekwa kwenye Pool C inayoaminika kuwa ngumu katika mashindano ya 2026 HSBC SVNS World Championship yatakayosakatwa tarehe 17-19 mwezi huu jijini Hong Kong.
Mashindano hayo yaliyo na timu 12 zilizogawanywa kwenye makundi 3, yatazikutanisha timu 8 kutoka Division 1 na 4 kutoka Division 2, ambako Shujaa walimaliza wa pili.
Mtanange huo unatarajiwa kuwa wa kufa kupona kwa Shujaa, wanapolenga nafasi ya kurejea katika Division 1 ya raga ulimwenguni.
Katika Pool C, kikosi cha Kenya kinakodoleana macho na Australia, New Zealand na USA, ambao ni miamba wa raga ulimwenguni.
Australia ilimaliza ya tatu katika Division 1, ingawa Shujaa waliwahi kuwakaba kwa sare ya 19-19 Dubai na kuwalaza 12-10 katika mashindano ya Perth.
New Zealand waliomaliza wa 4, wanasalia kuwa tishio kwa Shujaa, baada ya kuwakaranga mara 2 katika mashindano ya Perth.
Pambano kati ya Kenya na USA yatakuwa marudiano ya mikondo 3 ya HSBC SVNS Division 2, Kenya ikishinda mkondo wa mwisho wikendi iliyopita 31-14, ingawa USA walimaliza wa kwa jumla.
Mikondo mingine ya Championship itasakatwa katika mjiji ya Valladolid nchini Uhispania, na Bordeaux nchini Ufaransa.
Imetayarishwa na Antony Nyongesa
English 




























































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































































